Uncategorized

MAMBO MATATU TUNAYOJIDANGANYA ZAIDI KUHUSU FURAHA NA MAFANIKIO MAISHANI

Posted on

Ili uwe na maisha mazuri, ni lazima utapitia maisha magumu, yenye mabalaa na misukosuko, bila kujali neno mafanikio au ‘maisha mazuri’ kwako linamaanisha nini. Hutaweza kuishi maisha mazuri mpaka utakapopata ujasiri wa kuweza kuwa mkweli na nafsi yako. Si lazima kuwa mkweli kwa nafsi yako kwa asilimia mia moja, lakini kila unapozidi kuwa mkweli kwa nafsi yako ujue wazi kwamba unazidi kuyasogelea malengo uliyojiwekea.
Watu wenye “mafanikio ” huwa wanazungumza na nafsi zao mara kwa mara – mazungumzo yanayolenga kumnyoosha mustakabali wa maisha yao kuyaelekea malengo waliyojiwekea, na katika mazungumzo haya ya mtu na nafsi yake – wengi wanabaini uongo, na kauli zenye ukweli nusu wanazojiambia wenyewe.
Hakuna anayeweza kuotea mafanikio yanamaanisha nini kwako, lakini kama unaona umekwama kwa sasa, yawezekana kabisa ukawa unakwepa ukweli wa maisha kwa namna moja ama nyingine. Hujayaangalia maisha yako kiundani na kuanza kuihoji nafsi yako.
Zifuatazo ni baadhi ya kauli tunazojiambia ili kujiridhisha na hali tulizonazo hata kama hazituridhishi au tungetamani kuwa kwenye hali ya juu zaidi ya tuliyonayo sasa:
1. Nikipata “x” nitajisikia “y”
Ni jambo gumu sana kuamini kwamba una kila kitu unachohitaji ili kukufanya uwe mwenye maisha ya furaha na ni rahisi sana kujikuta umeingia kwenye mtego wa kufikiria kwamba mafanikio yako yanayofata yatakufanya ujisikie vizuri zaidi. Unajidanganya.
Mafanikio ni matokeo yanayokuja kwa wewe kuridhika kwakuwa unafanya shughuli unayoipenda kutoka moyoni. Mafanikio hayaendi kwa mtu anayefanya kinyume cha hayo (kwa asiyeridhika au kwa anayefanya shughuli asiyoipenda kwa dhati). Hii ni moja ya njiapanda kuu kabisa kimaisha.
Linapokuja swala la maisha yako, bila shaka unafikiria kwamba yanahitaji kurekebishwa kwakuwa kuna jambo haliendi sawa. Unadhani kwamba kuna jambo tofauti na wewe linalohitaji kurekebishwa ili ujisikie vizuri.
Mabadiliko yanatakiwa yaanzie ndani kuja nje (kwamba wewe mwenyewe ndio ubadilike kwanza ndipo uwaze kubadili mambo ya nje). Kuna baadhi ya hatua unazotakiwa kuchukua kwa kiasi kikubwa, mabadiliko yanatokea pale unapobadili mtazamo wako na nini unachohitaji uwe na furaha, ambacho si kingine bali utashi wako mwenyewe.
2. Nataka/naomba ‘x’
Sisi sote ni wabinafsi. Kila mmoja anataka mafanikio, furaha, pesa nyingi, uhuru na muda, mapenzi, afya nzuri — na kila kilicho kizuri maishani, tunakitaka. Kutaka yote haya si vibaya na haiepukiki, lakini kudhani kwamba yanatakiwa yashushwe kwako na wewe uanze kufaidi itakusababishia msongo wa mawazo hasa pale utapoyakosa.
Mara nyingine ukiulizwa swali kwanini unaona unastahili jambo fulani, unaweza kujikuta ukakwama na kushindwa kutoa jibu la kushawishi.
Unasema kwamba unastahili kupata mafanikio na utajiri — kwanini? Nini ulichofanya kinachokupa uhakika kwamba unastahili mafanikio na utajiri huo? Umefanya kazi kwa muda gani kuhakikisha lengo hilo linatimia? Umeyafanyia kazi malengo hayo?
Unadhani kwamba unastahili uhusiano mzuri na wenye utulivu — kwanini? Unaishi vipi na watu wengine? Ni kwa kiasi gani umeweka juhudi kuhakikisha tabia na mienendo yako inaweza kukubalika na watu wa aina unayopenda kuanzisha uhusiano nao badala ya kutaka watu wengine waendane na matakwa na tabia zako?
Haiwezekani kwenda benki kutoa pesa kabla ya kwanza kufungua akaunti na kuweka pesa zako kwenye akaunti hiyo – huu ndio utaratibu wa kimaisha. Huwezi kutarajia kupokea faida tu kama wewe mwenyewe hukufanya uwekezaji kabla. Utakapojua ukweli juu ya hili hutapata tabu unapokosa kitu. Usipoujua ukweli huu au kuamua kuudharau, basi kila mara utaona unaonewa au kutaka kila mtu awe anakutimizia mahitaji yako wewe tu.
3. Mpaka nilipofikia sasa, hakuna ninachoweza kufanya tena
Kuna wengine wanaweza kuona kwamba wamechelewa sana kufanya maamuzi katika ujana wao mpaka walipofikia sasa wanajiona wamechelewa. “Kwa sasa nina miaka 50, sio kijana kama wewe. Ningekuwa na nguvu ningeweza kufanya hayo unayosema, sasa hivi umri umeshakwenda sana.” Kauli kama hizi tumeshazisikia sana na ni kauli zenye uzito.
Lakini kuna mambo mawili yanasahauliwa au watu wenye umri kama huu wanashindwa kuyazingatia. Kwanza ni kwamba inaonesha kuwa tayari wameshakata tamaa kwenye maisha yao. Kana kwamba kufikisha miaka 50 ni sawa na kuvuka mstari wa mwisho kwenye mbio za marathon, kila kitu kinatakiwa kufikia tamati na kuanza kuhuzunika juu ya fursa ambazo ulishindwa kuzitumia maishani.
Pili ni watu wa umri huu kushindwa kujiuliza swali la msingi sana, kwa sasa nina miaka 50 – vipi ikiwa nitajaliwa umri mrefu na kuishi miaka 40 zaidi, maisha yangu yatakuwaje? Labda ukiona kwamba yawezekana ukawa na muda wa kuishi zaidi ndio utajua kwamba inabidi uweke mipango thabiti na kuanza kuitekeleza – bila kujali umechelewa kiasi gani.

from Blogger http://ift.tt/2iiC6Ca
via IFTTT

MAGHOROFA YA LUGUMI KUPIGWA MNADA NA SERIKALI

Posted on

Kampuni ya Udalali ya Yono imetangaza kupiga mnada majengo matatu ya ghorofa yanayomilikiwa na Kampuni ya Lugumi Enterprises Limited baada ya mmiliki wake kushindwa kulipa kodi anayodaiwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Agosti 20 mwaka huu katika gazeti la Sunday News lilitolewa tangazo la mnada wa majengo hayo ambayo ni mali ya Lugumi yanayotarajiwa kupigwa mnada Septemba 9 mwaka huu. Ghorofa moja lipo eneo la Upanga na kwa mujibu wa tangazo hilo, jengo hilo linafaa kwa ofisi na makazi, na majengo mawili ya Mbweni JKT yanafaa kwa makazi.
Scholastica Christian Kevela ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Yono alisema kuwa miezi minne iliyopita nyuma walifungia mali za Lugumi wakimtaka alipe malimbikizo ya kodi aliyokuwa akidaiwa, lakini hadi sasa hajafanya hivyo.
Kiongozi huyo wa Kampuni ya Udalali ya Yono ambayo ni wakala wa serikali wa kukusanya kodi kwa wadiwa sugu ambapo hushirikiana na TRA alisema mdaiwa huyo hajalipa mabilioni ya kodi anayodaiwa na hivyo wao wamepewa amri halali ya kuzipiga mnada nyumba hizo wananzozishikilia.
Kevela alikataa kutaja kiwango cha fedha ambacho Lugumi anadaiwa na TRA akabaki akisisitiza kwamba ni mabilioni ya shilingi na kwamba TRA ndio wanajua kiwango halisi. Hata hivyo hakutangaza thamani ya majengo hayo akisema kwamba, kila mtanzania aje na fedha aliyonayo kwani wao kama madalali hawana kiwango maalum.
Aidha, Kevela aliwataka wananchi kulipa kodi bila shuruti kuepuka nyumba zao kupigwa mnada huku akisema kwamba wasipofanya hivyo na deni lao likafika kwa Yono, wao watafanya kazi yao kiukamilifu.

from Blogger http://ift.tt/2v5vAkj
via IFTTT

MAZAO MATANO YANAYOINGIZIA SERIKALI FEDHA ZA KIGENI ZAIDI

Posted on

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali imeamua kufufua mazao matano ambayo yanaingiza kwa wingi fedha za kigeni nchini.
Amesema mbali ya korosho, Serikali imeamua kuboresha mazao ya tumbaku, chai, kahawa na pamba.
Ametoa kauli hiyo kwa nyakati tofauti jana na leo wakati akiwahutubia wananchi kwenye maeneo mbalimbali akiwa katika ziara ya kikazi ya siku nne mkoani Tabora.
Alisema kuanzania sasa serikali imepiga marufuku matumizi ya dola za Marekani kwenye ununuzi wa zao la tumbaku kwa sababu mazao mengine makuu hapa nchini yananunuliwa kwa fedha za Kitanzania.
“Ni kwa nini tumbaku inunuliwe kwa dola za Marekani ilhali mazao mengine yananunuliwa kwa fedha za Tanzania? Korosho, pamba, chai na kahawa wakulima wetu kote huko wanalipwa kwa fedha za Tanzania, kwa nini tumbaku iwe tofauti?” alihoji.
Alisema wenye makampuni wanaweza kukaa kwenye vikao vyao na kupanga bei zao kwa dola za Marekani lakini pindi wanapoingia nchini, watalazimika kufanya malipo kwa kutumia fedha ya Tanzania kwani mfumo malipo kupitia dola za Marekani umekuwa ukiwaibia wakulima kwa muda mrefu.
Waziri Mkuu amewataka watendaji na watumishi wa Halmashauri na wilaya za mkoa wa Tabora wasimamie zao la tumbaku ili kuinua kilimo cha zao hilo na kuwanufaisha wakulima.
“Maafisa kilimo na maafisa ushirika mnapaswa kulisimamia zao hili na siyo kuwaachia maafisa wa makampuni yanayonunua tumbaku.” 
“Kwa muda mrefu mlizembea na kuwaachia maafisa wa makampuni ya ununuzi ndiyo washughulike na wakulima. Nataka mbadilike, kuweni karibu na wakulima na muwasaidie kulima kisasa na kwa kutumia pembejeo,” alisema.
“Wasaidieni wakulima watoke kwenye mfumo wa kukopa pembejeo, wahimizeni wajiwekee akiba ili msimu ukianza wawe na fedha ya kununua pembejeo. Wakulima wanalaliwa sababu ya mikopo ya pembejeo. Makato yanakuwa mengi kiasi kwamba mkulima ahambulii chochote,” alisema.
Waziri Mkuu anaendelea na ziara yake wilayani Kaliua ambako atazungumza na wananchi.
IMETOLEWA NA: 
OFISI YA WAZIRI MKUU, 
IJUMAA, AGOSTI 11, 2017.

from Blogger http://ift.tt/2w0kws1
via IFTTT

RAIS MAGUFULI AKUTANA NA TAJIRI NAMBA MOJA DUNIA

Posted on

Taasisi ya Bill and Mellinda Gates imetenga Dola za Marekani Milioni 350 sawa na takribani Shilingi Bilioni 777.084 za Tanzania kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali katika sekta ya kilimo, afya na mifumo ya kielektroniki ya upatikanaji wa taarifa.
Mwenyekiti Mwenza wa taasisi hiyo Bw. Bill Gates amesema hayo leo tarehe 10 Agosti, 2017 Ikulu Jijini Dar es Salaam muda mfupi baada ya kufanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli.
Bw. Bill Gates amesema kama ambavyo taasisi yake imeshirikiana na Tanzania kwa kiasi kikubwa katika kuimarisha huduma za afya hapa nchini, fedha hizo zitaelekezwa katika utekelezaji wa miradi zaidi ya afya ikiwemo kupunguza vifo vya uzazi, kukabiliana na ugonjwa wa malaria, kuimarisha lishe na kukabiliana na utapiamlo, zitaelekezwa katika sekta ya kilimo ambako zitasaidia kuongeza uzalishaji wa mazao, kuzalisha mbegu bora na kuboresha ufugaji utakaoongeza chakula na pia zitasaidia kuweka mifumo ya kisasa ya upatikanaji wa taarifa.
Bw. Bill Gates ameelezea kufurahishwa na maendeleo ya uchumi wa Tanzania pamoja na uongozi na msimamo wa Rais Magufuli juu ya kutaka miradi hiyo ilete matokeo yenye manufaa, na amesema atakuja Tanzania mara nyingi ili kuimarisha zaidi ushirikiano na kufuatilia utekelezaji wa miradi.
Kwa upande wake Mhe. Rais Magufuli amemshukuru Bw. Bill Gates kwa mchango mkubwa unaotolewa na taasisi ya Bill and Mellinda Gates katika miradi mbalimbali hapa nchini ikiwemo fedha ambazo taasisi hiyo itazitoa katika kipindi cha miaka mitano kuanzia sasa na amemhakikishia kuwa Serikali yake itahakikisha fedha hizo zinaleta matokeo yaliyokusudiwa.
Mazungumzo kati ya Mhe. Rais Magufuli na Bw. Bill Gates yamehudhuriwa na Waziri wa Kilimo, Ufugaji na uvuvi Dkt. Charles Tizeba na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu.
Wakati huo huo, Mhe. Magufuli amekutana na kufanya Mazungumzo na Kaimu Balozi wa Marekani hapa nchini Mhe. Dkt. Inmi Patterson ambaye amesema Marekani itatoa fedha za nyongeza kiasi cha Dola Milioni 225 sawa na Shilingi Bilioni 499.500 za Tanzania katika mwaka ujao kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo itakayogusa sekta za elimu, afya, lishe bora, utawala bora.
Mhe. Inmi Patterson amesema Marekani imeongeza fedha hizo katika miradi inayotekelezwa hapa nchini kwa sababu ina dhamira ya dhati ya kushirikiana na Tanzania na itahakikisha uhusiano na ushirikiano huu unaendelezwa na kukuzwa zaidi.
Kwa upande wake Mhe. Rais Magufuli amemshukuru Mhe. Balozi Inmi Patterson kwa mchango mkubwa ambao Marekani imekuwa ikiutoa kwa Tanzania na amemhakiki kuwa Serikali ya Awamu ya Tano itaendeleza na kukuza zaidi ushirikiano wake na Marekani, na pia amemuomba awahimize wafanyabiashara na wawekezaji wengi zaidi wa Marekani waje kuwekeza na kufanya biashara hapa nchini kutokana na fursa lukuki zilizopo.
Mhe. Rais Magufuli pia ameiomba Marekani kusaidia kujenga hospitali kubwa ya kitaifa katika makao makuu ya nchi Mkoani Dodoma ili kuongeza uwezo wa Mkoa huo kutoa huduma za matibabu ikilinganishwa na ilivyo hizi sasa.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
10 Agosti, 2017

from Blogger http://ift.tt/2vSW1h6
via IFTTT

MAJINA 7 YA WAHALIFU WALIOHUSIKA NA MAUAJI YA ASKARI 8 WILAYANI KIBITI

Posted on

Tarehe 09.08.2017 majira ya saa 21:00 Hrs (saa tatu  usiku) katika mapori ya kijiji cha Rungungu mtuhumiwa akiambatana na Askari Polisi alikwenda kuonyesha Ngome ya watuhumiwa wenzake aliokuwa anashirikiana nao kufanya uhalifu.
Baada ya kukaribia eneo la tukio ulitokea upinzani mkali wa majibizano ya risasi jambo lililopelekea hata Abdallah Abdallah Mbindimbi @Abajani kujeruhiwa na risasi sehemu mbalimbali za mwili wake.
Kufuatia majibizano hayo, Askari Polisi walifanikiwa kuwajeruhi wahalifu 12 (kumi na mbili. Jitihada zilifanyika kuwapeleka Hospitali majeruhi wote 13 (kumi na tatu) ingawa baadae walifariki dunia kwa nyakati tofauti wakipelekwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kutokana na kuvuja damu nyingi zilizosababishwa na majereha ya risasi sehemu mbalimbali za miili yao. Miili ya marehemu imehifadhiwa kwenye chumba cha kuhifadhia maiti Hospitali ya Taifa ya Muhimbili Jijini Dar es Salaam.
Ndugu Wanahabari
Watuhumiwa 7 (Saba) kati ya 13 (kumi na tatu) waliopoteza maisha  kutokana na majibizano ya risasi wametambuliwa kuwa ni:
  1. Hassani Ali Njame
  2. Abdallah Abdallah Mbindimbi @ Abajani
  3. Saidi Abdallah Kilindo
  4. Abdulshakuru Mohamed Ubuguyu
  5. Issa Mohamed Mseketu @Mtawa
  6. Rajabu Thomas @Roja
  7. Mohamed Ally Kadude @Upolo
Miili 6 (sita) iliyobaki haikuweza kutambulika mara moja hivyo utambuzi utaendelea huko ilikohifadhiwa Hospitalini Dar es Salaam.
Ndugu Wanahabari
Vielelezo mbalimbali vilipatikana katika eneo la tukio, kama ifuatavyo:
S/N KIELELEZO UTAMBUZI
SILAHA, RISASI NA MABOMU
1. SMG = 5 Mali ya Jeshi la Polisi tukio la kupora Silaha Askari huko Mtengeni – Jaribu Mpakani
2. Anti Riot Gun 38mm = 2 Mali ya Jeshi la Polisi tukio la kupora Silaha Askari huko Mtengeni – Jaribu Mpakani
3. SAR = 1 Mali ya Jeshi la Polisi tukio la kupora Silaha Askari Polisi huko Stakishari Jijini Dar es Salaam
4. MAGAZINI = 2 Mali ya Jeshi la Polisi tukio la kupora Silaha Askari huko Mtengeni – Jaribu Mpakani
5. Risasi za SMG 158 Mali ya Jeshi la Polisi tukio la kupora Silaha Askari huko Mtengeni – Jaribu Mpakani
6. Bomu la kurusha kwa mkono = 1 Uchunguzi dhidi ya Bomu hilo unaendelea
7. Mabomu ya kutuliza ghasia = 4 Mali ya Jeshi la Polisi tukio la kupora Silaha Askari huko Mtengeni – Jaribu Mpakani
VIELELEZO VINGINE
8. Pikipiki  = 2 Pikipiki hizi zilitumika kuwasafirisha wahalifu hawa kwenye utekelezaji wa matukio ya uhalifu maeneo mbalimbali
9. Vitenge na Nguo mbalimbali Vitenge na nguo mbalimbali viliporwa baada ya kufanya tukio la kumuua Diwani wa Zamani wa Kibwiwi
10. Begi = 1 Liliporwa baada ya kumuua Mtendaji wa Kijiji cha Mangwe
Ndugu Wanahabari
Kwa mujibu wa taarifa za utambuzi wa vielelezo vilivyopatikana eneo la tukio na utambuzi wa baadhi ya miili ya watuhumiwa waliofariki  inaonyesha kuwa walishiriki matukio ya uhalifu maeneo mbalimbali kama ifuatavyo:
  1. Kuua OC CID na Watumishi 2 (Wawili) wa Idara ya Maliasili katika tukio la Jaribu Mpakani – Wilaya Kibiti
  2. Kuua Askari Polisi 8 (Nane) katika tukio la Mkengeni – Wilayani Kibiti
  3. Kuua Trafiki 2 (Wawili) katika tukio la Bungu “B” – Wilaya ya Kibiti
  4. Kumuua Diwani wa Zamani CCM katika tukio la  Kibwibwi – Wilaya ya  Kibiti
  5. Kuua Afisa Mtendaji,  Mwenyekiti wa Mtaa na Mkulima katika tukio la Kijiji cha Mangwi – Wilaya ya Kibiti
Ndugu Wanahabari
Wito wangu kwa Wananchi ni kuhusu mambo muhimu yafuatayo:
  1. Wananchi wote nchini kuondoa hofu ya kwamba eneo hili si salama. Nawaomba wananchi waendelee kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi na kwa kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu. Aidha nawaomba wananchi kutoa taarifa mara moja kwa Jeshi la Polisi  wanapohisi kuna jambo lolote wanalolitilia mashaka.
  2. Natoa wito kwa wananchi wa mkoa wa Pwani, hususani maeneo ya Mkuranga, Kibiti na Ikwiriri, kuendelea na shughuli zao mbalimbali za kujiletea maendeleo. Nawasihi kwa dhati kabisa waendelee kutupatia taarifa zitakazosaidia kumaliza kabisa uhalifu kwenye eneo hili. Nitumie fursa hii kuwashukuru sana wananchi wa maeneo ya Mkuranga, Kibiti na Ikwiriri kwa ushirikiano mnaotupatia ambao umesaidia sana kuwadhibiti wahalifu.
  3. Mamlaka za Hospitali, Zahanati, Vituo vya Afya, Maabara za Afya ya Binadamu na Maduka ya Kuuza Dawa za kutibu Binadamu zijiepushe na utaratibu wa kutoa matibabu kienyeji au kificho kwa watu waliojeruhiwa bila kufuata taratibu za kisheria ikiwemo kupata taarifa ya Polisi “kupitia Fomu maalum ya kuruhusu matibabu (maarufu kama PF. 3)”. Wahalifu wakijeruhiwa ni lazima watafute matibabu.
Kwa hiyo idara hizi ni muhimu sana kutoa ushirikiano ili kutuwezesha kuwakamata watuhumiwa maana baadhi yao wamekutwa na majeraha sehemu mbalimbali za miili yao na walikuwa wanaendelea kujitibia kwa kificho kwa kutumia dawa za hospitali.
Natoa wito kwa Mamlaka hizo kutoa taarifa mara moja kwa Jeshi la Polisi wanapoona ama kumbaini mtu ambaye ataonekana kuwa na majeraha na anatafuta tiba bila ya kufuata taratibu.
Ndugu Wanahabari
Napenda kuujulisha Umma kwamba wapo baadhi ya Watuhumiwa, Wafadhili na Washirika wa Uhalifu na Wahalifu wa ujambazi maeneo haya ambao bado hawajakamatwa. Jambo la kufurahisha ni kwamba taarifa zao zipo kwa Jeshi la Polisi nchini na zinaendelea kufanyiwa kazi ili  waweze kukamatwa na kufikishwa kwenye mkono wa Sheria mara moja.
Natoa wito kwa wananchi ambao wanawafahamu watuhumiwa wafuatao kutoa taarifa katika kituo chochote cha Polisi ili waweze kukamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria.
Picha za watuhumiwa hao zitasambazwa kote nchini ili iwe rahisi kuwabaini. Majina ya watuhumiwa hao ni:
i.Anafi Rashid Kapelo @ Abuu Mariam
  1. Hassan Haruna Kyakalewa @ Abuu Salma @ Shujaa @ Dokta
iii.  Haji Ulatule
  1. Shekhe Hassan Nasri Mzuzuri
  2. Rashid Mtutula
Ndugu Wanahabari
Nimalizie kwa kusema kwamba uhalifu kwenye eneo hili ni suala la muda mfupi. Na tunaendelea vizuri sana. Hali ya usalama imeimarika sana eneo hili. Nazidi kutoa wito kwa wananchi kuendelea kuliunga mkono Jeshi la Polisi ili kufikia malengo yake ya kuzuia, kubambana na kutanzua uhalifu nchini.
 
Imetolewa na;
Simon Nyakoro Sirro
Inspekta Jenerali wa Polisi
IKWIRIRI
10.08.2017

from Blogger http://ift.tt/2useYXE
via IFTTT

MASKINI…Mwanamke Aolewa Saa 10 Jioni, Afariki Saa 7 Usiku na Kichanga Tumboni…..

Posted on

DAR ES SALAAM: Hii inauma sana! Wakati wengi wakitamani kuingia kwenye ndoa ili kuyafurahia maisha hayo, kwa binti Zai Mkiwa, mkazi wa Mtoni Kijichi jijini hapa, imekuwa tofauti kwani amejikuta akiyaonja maisha ya ndoa kwa saa chache na kisha kufariki, Amani linakudadavulia habari hii ya kusikitisha.
TUJIUNGE NA CHANZO
Kwa mujibu wa chanzo makini kilichohudhuria msiba wa binti huyo, Zai ambaye alidaiwa kuwa na ujauzito mchanga, alionekana ni mwenye siha njema hadi siku ya harusi, Jumapili iliyopita (Julai 30, mwaka huu) kabla ya kukutwa na umauti usiku wa saa 7 siku hiyo.
“Yaani marehemu alikuwa na afya njema kabisa, na siku ya harusi yake hakuonesha hata dalili zozote za kuumwa japo kuna wakati alisema anahisi kama kuishiwa nguvu.
FULL KUTABASAMU
“Muda mwingi alikuwa akitabasamu, alifurahia ndoa yake kwelikweli kama unavyojua watoto wa kike wanavyofurahia siku hiyo muhimu katika maisha yao,” kilisema chanzo hicho.
NDOA ILIFUNGWA SINZA MAPAMBANO
Kikizidi kufunguka chanzo hicho kilieleza kuwa, siku ya tukio, mumewe aliyefahamika kwa jina moja la Yasin, alifika nyumbani kwa babu wa marehemu, Mzee Msafiri anayeishi Sinza Mapambano jijini hapa na kukamilisha taratibu zote za ndoa na baada ya zoezi hilo kukamilika, Zai aliambatana na mumewe kwenda nyumbani kwao, Mtoni Kijichi.
…Hali ilivyokuwa siku ya harusi yake.
“Huwezi amini kumbe ni kama alikuwa anatuaga vile, maana tumesherehekea pale kwa nderemo na vifijo, wakaondoka zao na mumewe lakini ilipofika saa 7 usiku, tunaambiwa amefariki dunia,” kilisema chanzo hicho.
ALIANZA KUTAPIKA
Chanzo hicho kilieleza kuwa, ndugu wa karibu na marehemu walipopewa taarifa za msiba huo, walielezwa kuwa Zai alipofika nyumbani kwa mumewe, saa chache kabla ya kukata roho, alianza kutapika na mumewe akamkimbiza Hospitali ya Mbagala Zakhem lakini bahati mbaya, alifariki.
“Walifika salama salmini, wakahifadhi zawadi mbalimbali walizokuwa wamepewa na kisha kulala. Ilipofika saa saba usiku nasikia ndiyo akaanza kutapika na mumewe alipoona hali inazidi kuwa mbaya akalazimika kumkimbiza hospitalini, lakini alipofikishwa tu akafariki akiwa mikononi mwa madaktari,” kilisema chanzo hicho.
MSIBA WAWEKWA ALIPOOLEWA
Chanzo hicho kiliendelea kuweka bayana kuwa, asubuhi ya Jumatatu, Julai 31, mwaka huu, ndugu walikusanyika nyumbani kwa babu wa marehemu, Sinza-Mapambano ambapo taratibu zote za msiba ikiwemo mazishi zilifanyika pale.
“Palepale tuliposherekea harusi ndipo tulipokusanyika tena kwa ajili ya msiba. Yaani lile turubai lililotumika katika sherehe ya harusi yake ndilo hilohilo lililotumika wakati wa msiba wake, inauma sana! Tukaomboleza pale na baadaye mida kama ya saa 10 jioni, mwili wa Zai ulienda kuzikwa katika Makaburi ya Sinza,” chanzo kilizidi kueleza.
NI NDANI YA MASAA 24 TU!
Ukweli ni kwamba, mambo yote hayo yametokea harakaharaka mno, ni ndani ya saa 24 tu! Kila kitu kwenye maisha ya binti huyo kikabaki kuwa historia ya majonzi na masikitiko kwa ndugu na jamaa waliobaki duniani.
MUMEWE ABAKI NA MACHUNGU
Kwa mujibu wa chanzo hicho kilisema kikiwa makaburini hapo, mume wa marehemu alionekana kama mtu aliyepigwa na bumbuwazi, haamini kwa kilichotokea, hajielewielewi kwani hata kuzungumzia undani wa mazingira ya kifo cha mkewe hakuweza.
KABLA YA NDOA ALIUMWA
Inasemekana, siku chache kabla Zai hajaolewa, aliishiwa nguvu na kukimbizwa hospitali lakini alitibiwa na kurejea nyumbani na hata ilipofika siku ya harusi, alikuwa mzima wa afya.
BABA AZUNGUMZA
Gazeti la Amani lilifanikiwa kuzungumza na baba wa marehemu, Ketel Madua ambaye alisema amepokea kwa masikitiko makubwa kwa kuondokewa na binti yake huyo, saa chache baada ya kumuoezesha. Gazeti hili linatoa pole kwa ndugu na jamaa kwa msiba wa Zai.

from Blogger http://ift.tt/2v3iC9e
via IFTTT

Facebook Wataanza Kulipa Watu Kupitia Video Wanazopakia kwenye mtandao huo

Posted on

Facebook wapo mbioni kuhakikisha watu wanaanza kulipwa kwa kupakia video na maudhui mengine kwenye mtandao huo, ambapo hivi karibuni wameinunua kampuni ya masuala ya hakimiliki mtandaoni Source 3 ili kuhakikisha hakuna wizi wa maudhui yatakayokuwa yanapakiwa kwenye mtandao huo, ikiwa pamoja na kuzuia watu watakao kuwa wana nakili maudhui ya watu wengine ili kujiingizia pesa kupitia matangazo yatakayokuwa yanatokea wakati video au kitu chochote kikiwa kinatazamwa na mashabiki wa mpakiaji.
Source 3 watakuja na teknolojia ambayo inafanya kazi sawa na ile inayotumika kwenye YouTube inayofahamika kama YouTube Content ID. Teknolojia hiyo itawawezesha wapakiaji video kwenye Facebook kuweza kuzuia video zao zisipakiwe na watu wengine au kuchukua mapato yatakayopatikana kwenye video hiyo kutoka kwa mtu ambaye si mmiliki halali wa video.
Pia Facebook walizindua app maalumu kwa wamiliki wa kurasa. App hiyo itawawezesha wamiliki wa kurasa kwenye mtandao huo kuweza kuwapatia mashabiki wao machapisho ya kwenye kurasa zao moja kwa moja huku wakitengeneza pesa kupitia machapisho hayo.
Kwa sasa Facebook inazaidi ya mashabiki bilioni 2 ambao kila mwezi lazima waingie kwenye mtandao huo, Facebook inatarajiwa kuwa ndiyo sehemu kubwa ya kuingiza pesa kwa watu watakaokuwa wanamiliki kurasa kwenye mtandao huo, huku YouTube ikishika mkia.

from Blogger http://ift.tt/2wrx6xe
via IFTTT

TAZAMA Dunia Yetu Ilivyo Ndogo Ukilinganisha Na Sayari Zingine

Posted on

Dunia yetu inaonekana ni kubwa sana ambapo ukubwa huo unatufanya sisi tujione ni wadogo sana. Ni kweli Dunia yetu ni kubwa sana ukilinganisha na sisi, lakini tukiangalia upande wa pili na tukailinganisha na sayari au vitu vingine ulimwenguni basi lazima utastaajabu kuona jinsi gani sisi na Dunia yetu tulivyowadogo sana.
Kutokana na kukua kwa teknolojia siku hadi siku wanasayansi wameweza kuziona sayari, nyota na vitu vingine vilivyokuwa mbali sana kupitia darubini kubwa zilizokuwa huko angani. Picha zifuatazo zitakuonesha ni jinsi gani Dunia yetu ilivyokuwa ndogo ukilinganisha na vitu vingine vilivyokuwa huko angani.
Hii inafahamika kama SuperCluster of Galaxies au muunganiko wa galaksi mbali mbali kitaalamu inaitwa Laniakea (Mbingu isiyopimika). Hapo mshale ulipoonyesha ndipo galaxy yetu inayoitwa Milky Way ilipo.
Hapo mshale ulipoelekeza ndipo galaksi ya Milky Way ilipo
Kama tukiikuza picha ya SuperCluster kwa ukaribu kuelekea kwenye galaxy yetu ya Milky Way hivi ndivyo itakavyoonekana kwa ukaribu. MilkyWay ndiyo galaxy yetu tulipo sisi, hapo kwenye mshale ulipoelekeza ndipo Jua letu, Dunia, pamoja na Sayari zingine zote zilizokuwa kwenye mfumo wetu wa Jua zilipo. Hivyo vidoti vyenye rangi mbali mbali vinavyong’aa ndizo nyota zote tunazoziona usiku. Hapo kati kuna shimo jeusi (Black Hole) ambalo linafyonza hizo nyota zote ikiwemo na sayari zake kuingia humo ndani. Siku moja na sisi Jua letu litafika hapo baada ya miaka bilioni kadhaa huko mbele.
Hapo mshale ulipoelekeza ndipo mfumo wetu wa jua ulipo (Jua na sayari zote ikiwamo na dunia yetu)
Jua letu limechukua asilimia 99.86% ya sehemu yote kwenye mfumo wetu wa jua (Solar System) na ni kubwa sana ambapo Dunia milioni 1.3 zinaweza kutosha ndani yake.
Hapo mshale ulipolekeza ni dunia
Pete za kwenye sayari ya Zohali ni kubwa sana ambapo Dunia sita zinaweza kutosha kwenye pete hizo. Hizi pete ni mchanganyiko wa mapande makubwa ya barafu na mawe yanayozunguka sayari hiyo ya Zohali.
Dunia sita zinaweza kutosha kwenye pete ya zohali
Hilo doti kubwa jekundu unaloliona ni kimbunga kikubwa sana kilichomo katika sayari ya Sumbula. Kimbunga hicho ni kikubwa sana ambapo Dunia tatu zinaweza tosha.
Dunia tatu zinaweza kutosha kwenye kimbunga cha kwenye sayari ya Sumbula
Hii picha ilipigwa mwaka 2013 na chombo kinachoitwa NASA Cassin Spacecraft. Hicho kidoti cha bluu kilichooneshewa mshale mwekundu ni Dunia yetu. Umbali kutoka eneo picha hii ilipopigwa mpaka Duniani ni maili milioni 898.
Hicho kidoti cha bluu kilichooneshwa na mshale ni Dunia yetu

from Blogger http://ift.tt/2v3e9Dq
via IFTTT

RAIS MAGUFULI AANZA ZIARA YA SIKU 5 MKOANI TANGA

Posted on

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na wananchi wa Mkata wakati alipokuwa njiani kuelekea mkoani Tanga kwa ajili ya ziara ya kikazi.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli akiwapungia mkono wananchi wa Mkata waliosimama pembeni ya barabara kuu ya Chalinze- Segera (hawaonekani pichani) mara baada ya kumaliza kuhutubia katika kijiji cha Mkata mkoani Tanga.
Viongozi mbalimbali wa mkoa wa Tanga akiwemo Wabunge na wakuu wa Wilaya wakipiga makofi wakati Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli alipokuwa akihutubia Mkata mkoani Tanga.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na wananchi wa waliosimama pembeni ya barabara kuu ya Chalinze Segera katika eneo la Kwa mkonga wakati akiwa njiani kuelekea Tanga.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli akiwapungia mkono wananchi wa Kabuku mara baada ya kumaliza kuwahutubia wakati akielekea mkoani Tanga.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli akihutubia wakazi wa Kabuku Handeni mkoani Tanga.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martin Shigela kabla ya kuwahutubia wananchi wa Hale mkoani Tanga.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli akihutubia wakazi wa Hale mkoani Tanga.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli akisalimiana na mmoja ya wakazi wa Hale mkoani Tanga mara baada ya kuhutubia katika eneo hilo.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli akimpongeza Mwanachama wa Chama cha Mapinduzi CCM Hadija Juma mara baada ya kusoma ujumbe ulioandikwa kwenye sare aliyovaa mama huyo.
Wananchi wa Muheza wakimpokea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli mara baada ya kufika katika eneo hilo la mjini akiwa njiani kuelekea Tanga. PICHA NA IKULU.

from Blogger http://ift.tt/2v4Ysdj
via IFTTT

WANANCHI WAPEWA SHAMBA LA JKT NA RAIS MAGUFULI

Posted on

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amesema Serikali imeanza kuchukua hatua dhidi ya watu waliouziwa mashamba makubwa Mkoani Tanga na kisha kuyatelekeza ambapo mpaka sasa hati miliki za ardhi 5 zenye zaidi ya ekari 14,000 zimefutwa.
Mhe. Rais Magufuli amesema hayo leo tarehe 03 Agosti, 2017 kwa nyakati tofauti wakati akizungumza na wananchi wa Mkata, Komkonga, Kabuku, Michungwani, Hale, Muheza na Pongwe katika Wilaya za Handeni, Muheza na Tanga ambako ameanza ziara ya kikazi ya siku 5 Mkoani wa Tanga.
Mhe. Rais Magufuli amefafanua kuwa Mkoa wa Tanga una mashamba 72 yaliyouzwa kwa watu mbalimbali na kwamba hatua za kunyang’anya mashamba yaliyotelekezwa zimeanza kuchukuliwa kwa mashamba 12 na tayari mashamba 5 ambayo hati zake zimeshafutwa, utaratibu unaendelea kuwagawia wananchi na wawekezaji watakaokuwa tayari kuyaendeleza kama ilivyokusudiwa.
Sambamba na hilo akiwa Mkata Wilayani Handeni, Mhe. Dkt. Magufuli ameagiza shamba la ekari 50 lililopo katika kijiji cha Kabuku na ambalo lililotolewa na wananchi kwa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa lengo la kujenga kiwanda miaka 7 iliyopita, lirejeshwe kwa wananchi na ametaka JKT ijenge kiwanda hicho katika eneo lake jingine lenye ukubwa wa zaidi ya ekari 9,000.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli ametoa siku 15 kufanyika kwa uchunguzi wa fedha kiasi cha Shilingi Milioni 500 zilizotolewa kwa ajili ya ujenzi wa majengo ya kituo cha afya cha Mkata, kufuatia kuwepo kwa taarifa za ufujaji wa fedha hizo na ameongeza kuwa Serikali itapeleka Shilingi Milioni 800 kwa ajili ya kuendeleza kituo hicho baada ya hatua stahiki kuchukuliwa.
“Siku 15 tuwe tumepata jibu ili fedha nyingine Shilingi Milioni 800 zije, kama huyo Mkandarasi hafai afukuzwe, kama kuna mtu hafai aondolewe, tuanze na ukurasa mpya, na ningeomba Mkuu wa Wilaya ulifuatilie hili ili asiponyoke mtu yeyote, na wewe una Mamlaka yote” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Kuhusu maji, Mhe. Rais Magufuli amesema Serikali imeanza kuchukua hatua dhidi ya tatizo hilo ikiwemo kutoa Shilingi Bilioni 2 kwa ajili ya kuupatia maji Mji wa Muheza na vijiji vingine na kwamba mradi mwingine wa Shilingi Bilioni 30 utatekelezwa ili kumaliza tatizo hilo.
Mhe. Rais Magufuli amewataka wananchi wa Tanga kujipanga kunufaika na fursa mbalimbali za ajira na biashara kufuatia mradi mkubwa wa ujenzi wa bomba la mafuta ghafi la kutoka Hoima nchini Uganda hadi bandari ya Tanga hapa Tanzania na amewahakikishia kuwa mradi huo utatoa mchango mkubwa katika maendeleo ya Tanga na Taifa kwa ujumla.
“Ndugu zangu wananchi wa Tanga nataka kuwahakikishia kuwa tunakwenda vizuri, tumepata mradi huu mkubwa na pia uchumi wetu unakwenda vizuri, hivi sasa nchi yetu ni kati ya nchi 5 duniani zenye uchumi unaokua kwa kasi na ni nchi ya 2 barani Afrika ikitanguliwa na Ethiopia” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Katika ziara hii Mhe. Rais Magufuli ameongozana na Mkewe Mama Janeth Magufuli, Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira Mhe. Januari Makamba na Wabunge wa Mkoa wa Tanga.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Tanga
03 Agosti, 2017

from Blogger http://ift.tt/2uaw7F9
via IFTTT